KWA HABARI NA UCHAMBUZI WA UHAKIKA,KITAIFA NA KIMATAIFA,USIKOSE KUTEMBELEA BLOG HII.

Friday, December 25, 2015

UISLAMU PEKEE NDIO UNAOJALI FAMILIA

Na Suleiman Abdullah

Tarehe 15 Mei ya kila mwaka imetangazwa ni Siku ya Familia Duniani. Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa huiadhimisha siku hiyo inayotokana na Tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa No. 47/257 la tarehe 20/09/1993. Tamko hilo liliifanya siku hii kuwa maalum kwa ajili ya familia. Nchi zote duniani huiadhimisha siku hii kwa kujadili nafasi ya familia kwenye jamii na maendeleo kwa ujumla.
Cha kushangaza ! wanademokrasia wanaweka Siku ya Familia ilihali nidhamu ya kidemokrasia ndio mdau mkubwa wa kuvunja na kusambaratisha hizo familia. Kwa mfano, Ulaya imefikia mpaka mama na mtoto wanaishi kimkataba. Kwa hakika suala hili ni fedheha kubwa kwa mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kisiasa ya kidemokrasia.

Aidha, tunashuhudia namna fikra za kimaslahi, ukandamizaji wa kiuchumi wa mfumo wa ubepari unavyozipeleka mchamchaka familia kiasi kwamba hazina muda wa kuketi pamoja. Kwa sababu muda mwingi kutumia kazini au mashuleni. Karibuni mbunge Susan Lyimo (Viti maalumu Chadema) alitamka wazi kwamba msongamano wa magari jijini Dar-es Salaam unaanza kuleta migogoro ya ndoa ndani ya familia (Gazeti la Mwananchi. Uk 16. Mei 9, 20014) Kwa kuwa baba muajiriwa na mama nae kutokana na hali ngumu, fikra za kujiongezea, shinikizo la kiuchumi, fikra za uhuru wa mwanamke pia nae muajiriwa, na watoto wanasoma shule ya bweni. Mama akirudi kachoka na baba akirudi kachoka hawana muda wa kukaa pamoja. Na kwa watoto wasiosoma shule ya bweni wakirudi nao pia wana kazi za nyumbani (homework). Ikiwa vikundi hivi vitatu baba, mama na watoto hawana muda wa kuketi pamoja kufurahi na kuchanganyika pamoja kwa ajili ya ustawi wa kifamilia. Vipi tena watakuwa na muda wa kuwatembelea jamaa wengine wa karibu?

Na kwa upande wa fikra ya kimaslahi Ubepari/udemokrasia umeshindwa kuzifanya familia kuwa kitu kimoja. Kwani mfumo huu unalingania kila kitu kupimwa kwa mtazamo wa kimaslahi. Hata kumpenda mama, baba, dada nk. mtu huaangalia kwa jicho la maslahi fulani. Ndio maana ukaona ndugu humpenda dada, kaka au jamaa mwenye uwezo zaidi kifedha kuliko asiyekuwa na uwezo. Au pia wazazi nao humthamini zaidi mtoto mwenye kazi na fedha kuliko aliyekuwa hana kazi na uwezo. Kipimo cha maslahi kimeweza kuvunja na kusambaratisha familia nyingi sana. Tunashuhudia hata hapa petu kila siku familia zinagombana hata kwenye masuala madogo madogo kama mirathi hadi kufikia kutukanana matusi ya nguo na kupigana hadharani bila ya aibu wala fedheha na hatimae kuvunja udugu ambao ni kitu adhimu kutoka kwa Mola wetu Muumba.

Tusisahau pia fikra chafu nidhamu ya kidemokrasia za uhuru (freedoms). Yaani mtu kufanya alitakalo. Hakika ni kioja kikubwa kwa wanademokrasia kumlingania mwanadamu kwamba ana uhuru wa kufanya anavyojisikia. Fikra hizi ndizo zinazozalisha kila aina ya maovu kuanzia uzinifu, ulevi, usagaji, ushoga nk. Na kwa kuwa hawawezi kuyakhalifu yaliyozaliwa na fikra hizo, leo kwa upotofu mkubwa tafsiri ya familia imetanuliwa mpaka kuhusisha watu wa jinsia moja. Yaani kinachoitwa ndoa ya wanawake kwa wanawake na wanaume kwa wanaume. Subhannallah!

Hapana shaka maadhimisho ya Siku ya Familia na mithili yake hayana tija yoyote kwa Umma bali ni michezo ya kimaslahi wanayoiweka mabepari kujiongezea kipato kutokana na maandalizi ya matamasha na maonyesho mbalimbali ambayo bajeti zake hutunisha mifuko yao.

Uislamu ukiwa mfumo wa haki ndio unaojali familia kipindi chote na sio siku moja kwa mwaka. Aidha, umeikunjuwa dhana ya familia kwa upana sio mume, mke, watoto na mbwa wao ! Bali inahusisha jamaa wote, na ni haramu na dhambi kubwa kuwatupa.
Tunaona sera ya Uislamu jinsi gani unavyohimiza kutunza familia na kuiendeleza kupitia maamrisho na makatazo aliyoyaweka Allah Taala kwa viumbe vyake kupitia Mtume( SAAW). Yeye ametuhimiza, kutufundisha na kutushajiisha kutunza familia. Uislamu umetangaza wazi kwamba baba ni mchunga na ataulizwa kwa kile anachokichunga. Kauli hii pekee yatosha kuonyesha jinsi gani mzazi anapotakiwa kuwa karibu na familia yake ili kuipa huduma mbali mbali yakiwemo maadili mema. Na Allah Taala kutoa fursa ya kuoa mke zaidi ya mmoja ni dalili tosha kwamba wanaume wana uwezo wa kutunza familia. Na chini ya kivuli cha dola ya Kiislamu ya Khilafah mazingira ya kutunza na kusimamia familia yatasahilishwa zaidi ili kuhifadhi taasisi hiyo muhimu katika ustawi wa wanadamu

No comments: