UCHAGUZI MKUU TANZANIA: CCM na UKAWA Timu Mbili Chini Ya Kocha Wao Mmoja MAREKANI.
Mwandishi: Suleiman A Mbarouk
Ni wiki kadhaa sasa tokea maamuzi magumu yafanyike kumpata mgombea wa nafasi ya Uraisi kupitia CCM na CHADEMA (UKAWA).
Wanasiasa , wasomi , wafanyabiashara na raia wa kawaida wameshuhudia wasiyoyatarajia kuibuka kidedea kwa John Pombe Magufuli , msomi na Waziri wa Wizara ya Ujenzi kuwa mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM. Mgombea huyu hajawahi kushika hata nafasi ya mjumbe wa kata wa CCM.
Kwa upande mwengine , Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa , msomi , mfanyabiashara , mwanasiasa na rafiki mkubwa wa zamani wa Raisi anayemaliza muda wake Jakaya Mrisho Kikwete. Pia Lowassa akiwa ni mwanajeshi aliyewahi kupigana vita vya kumng’oa Iddi Amin Dada wa Uganda mwishoni wa miaka ya 70 ,aliibuka kidedea kuwa mgombea wa Uraisi wa Umoja wa Kutetea katiba ya wananchi –UKAWA kupitia chama cha CHADEMA.
Wengi bado wanashaka ya kulikoni na nini hatima ya Tanzania , nchi inayotawaliwa na CCM chama chenye ukomavu wa hali ya juu chama katika kutatua mifarakano ya ndani na umahiri wa viongozi wake. Je, kuna ufa wa ndani usiozibika ?
Udhaifu wa kuyumba kwa maamuzi ulijitokeza tokea wakati wa mchakato wa rasimu ya katiba mpya. Inasemekana Raisi Kikwete ambaye yeye na chama chake wapo upande wa Amerika alishayabariki maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Warioba ya serikali tatu ,30 Disemba 2013 katika viwanja vya Karimjee Dar Es Salaam http://mkwinda.blogspot.com/2014/03/.
Kwa mshangao wa wengi akaibeza rasimu hiyo hiyo , kwa kishindo katika ufunguzi wa Bunge la Katiba na kuja na ile iliyopendekezwa na chama chake tawala cha CCM ya kuendelea na mfumo wa muungano wa serikali mbili kwa msisitizo kuwa kati ya watu 351,664 waliotoa maoni ni 47,820 ndiyo waliojadili muundo wa muungano ambao ni sawa na 13.6% tu. Kwa kauli yake hiyo 86.4 % bado wanapenda waendelee na mfumo wa serikali mbili. Katika munasaba wa tukio hilo Kikwete alitoa hadithi yenye fumbo zito inayomuhusu mvuvi na jinni. Alisema “Mvuvi aliokota chupa baharini akidhani ndani yake muna mali. Alipoifunguwa chupa hiyo lilitoka jinni lililomshukuru mvuvi kwa kumfanya kuwa huru. Hata hivyo jinni huyo akamwambia mvuvi kuwa ana njaa kali, na chakula chake ni yeye. Mvuvi alipoona kitisho cha maisha yake akatumia hekma kwa kumwambia jinni, kuwa haamini kwa ukubwa alionao anaweza kuingia chupani ., Jini likaonyesha namna linavyoingia chupani . Kwa hafla, mvuvi akaifunga chupa na kuirembea baharini , kuokoa maisha yake”. Kiuhakiki wa lugha namna mambo yalivyotokea naweza kusema jinni lilikuwa CCM na mvuvi ni Kikwete.
Serikali za Ujerumani na Amerika zikatia shaka jinsi ya rasimu ya katiba ilivyopitishwa kwa nguvu katika Bunge la Katiba bila ya ridhaa ya wajumbe wa bunge hilo chini ya Mwenyekiti wake Samuel Sitta.
www.constitutionnet.org/.../report_on_the_tanzania_draft_constitution_.
Kasoro kubwa mojawapo ya kisiasa iliyojitokeza ndani ya CCM ni katika uteuzi wa mgombea uraisi kwa tiketi ya CCM. Wengi walitarajia wanasiasa waandamizi kama vile Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani Fredric Sumaye ,Makamo wa Raisi Dr Bilali, Jaji Augostino Ramadhani , Waziri wa mambo ya Nje Bernard Membe na Waziri Pr. Mark Mwandosya wawe miongoni mwa wateule wa tano bora. Kampeni ya kutafuta wadhamini ya wagombea wote hao inaonyesha kuwa Edward Lowassa ndiye anayekubalika kuliko wagombea wote . Lakini Kamati ya Maadili inayoongozwa na Maraisi wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Mkapa wakarudisha majina ya Bernard Membe , Januari Mkamba ,John Magufuli, Asha Rose Migiro na Amina Salum Ali na hatimae John Magufuli kuibuka mgombea wa Uraisi.
Hii ni sababu kubwa iliyomfanya Edward Lowassa, Sumaye na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali na wanachama kadhaa kutoka CCM na kujiunga na UKAWA ambao umepata nguvu katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu Oktoba 2015.
Kwa maoni yangu, mpambano uliopo ni wa timu mbili ambazo tayari zipo uwanjani chini ya kocha mmoja yaani Amerika kutokana na nukta zifuatazo:
Kwanza: Siasa za kisekula hazina rafiki wala adui wa kudumu bali zina maslahi ya kudumu. Kutokana na CCM na serikali yake kujipamba kwa ufisadi, wizi na rushwa , ni dhahiri sehemu kubwa ya umma lazima ujitenge nayo. Amerika haitopendelea ionekane imeshiriki katika maovu haya yaliyofanywa na vibaraka wake ingawaje nyuma ya pazia imehusika. Na hivi ndivyo ilivyowatelekeza vibaraka wake katika Arab Spring na kujiingiza katika wimbi la mageuzi , kuwaweka madarakani vibaraka wengine . Na huu ndio mchezo aliocheza kumuondoa Lowassa CCM kwa mkono wa Kikwete na kumpeleka UKAWA . Na hivi ndivyo ilivyotumika katika uchaguzi wa 2010, wakati mtu wake Kikwete alipokuwa na upinzani mkubwa ilimtumia mtu wake Lipumba wa CUF ili kura zake ziende kwa JK .Kwa hivyo, yoyote kati ya washindani wawili, Magufuli au Lowassa, atakayeungwa mkono na kushinda , Amerika bado itaendelea kuhodhi siasa za Tanzania. Na Uingereza lazima ikubali matokeo na itabakia kuwa kama fisi kungojea mfupa uanguke ipate sehemu yake , kama inavyofanya katika sehemu kadhaa zinazovamiwa na Amerika kama vile Iraq, Afghanistan nk.
Pili: CHADEMA ambacho ndicho kilichotoa mgombea wa Uraisi kupitia UKAWA kina mahusiano ( bilateral relations ) na chama cha Conservative cha Uingereza Lakini moja ya wafadhili wake wakubwa ni Konrad Adenauer Stiftung/KAS ya Ujerumani ambayo ni chama cha Christian Democrat cha Angela Mikel ambacho kina mahusiano makubwa na Amerika. Aidha, mshirika mkubwa wa UKAWA ni CUF ambacho kiasili kimeundwa na Amerika na viongozi wake wakuu ni vibaraka wa Amerika. Kwa hivyo, maslahi ya Amerika yatahifadhiwa ikiwa kutatokea wimbi la upinzani ndani yake. Na wimbi la viongozi wanaomuunga mkono Lowassa limesheheni CHADEMA kujizatiti zaidi kisiasa.
Na mwisho: Amerika inautangaza uchaguzi wa Tanzania iwe mjadala maalum kiulimwengu . Hili linathibitishwa na kipindi maalum cha “Hard Talk cha Voice of America cha ShakaSsali. Tayari mjadala umeshaanza juu mchakato wa uchaguzi Tanzania na kujenga hoja kwa ushahidi wa vipande vya filamu/clipps kuwa Edward Lowasa anakubalika zaidi.
Source: hizbestafrica.com
