KWA HABARI NA UCHAMBUZI WA UHAKIKA,KITAIFA NA KIMATAIFA,USIKOSE KUTEMBELEA BLOG HII.

Friday, August 14, 2015

Kutumia Jeshi Kiufisadi Ili Kubaki Kwenye Mamlaka



Na Kassim Agessa

Habari:

Katika gazeti la The Standard la Agosti 1, 2015, Roselyn Obala na Juma Kwayera waliandika kuwa, 'Jukumu la Jeshi la Kenya (KDF) katika usalama wa ndani inaweza kuongezeka kama mapendekezo katika mswada mpya yatakuwa sheria.

Mswada wa Marekebisho ya KDF 2015, ikipitishwa kuwa sheria, itampa mamlaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kupeleka KDF katika shughuli za kiraia. Hoja hi kwa kiasi kikubwa ni mabadiliko ya uendeshaji na amri iliyo kwa sasa mikononi mwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP). Vile vile, Katibu wa ulinzi katika baraza la Mawaziri hana jukumu kubwa katika kukabidhi majukumu ya kiraia kwa Mkuu wa Majeshi. Mswada huu ulioko katika hatua ya uchapishaji ina ishara ya muundo wa vikosi vya usalama katika Uganda, Rwanda, Ethiopia na Sudan, ambapo hakuna mpaka wazi katika upeo wa kazi za polisi na jeshi. Nchini Uganda na Ethiopia, kwa mfano, Jeshi ndio hutumika wakati wa uchaguzi kusimamia vituo vya kupigia kura.

Maoni:

Ingawa mswada wenyewe bado haujawekwa nje kwa uchunguzi, nia yake ni wazi kabisa. Kwa kuutazama mswada huu kwa haraka haraka unadhihirisha kuwa mapendekezo hayana ubaya wowote zaidi ya serikali kuhuisha shughuli za huduma zake za usalama ili kukabiliana na vitisho vya usalama. Hata hivyo, sababu za kimsingi zinaonyesha kuwa mswada huu hauna uhusiano wowote na kulinda nchi badala yake ni kuimarisha nguvu na kujenga vipenyezo  vya ufisadi mbali kabisa na macho ya ummah. Makala ya The Standard yanaendelea kueleza kuwa Mswada pia unalenga kuanzishwa kwa kikosi maalum cha akiba kinachojumuisha Huduma ya Kulinda Wanyamapori (KWS), Walinzi wa Misitu (KFS) na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kutumikia pamoja na KDF. "Rais anaweza katika hali ya dharura au maafa au wakati wa vita, au machafuko kuamrisha kikosi hiki cha Walinzi wa Misitu na NYS kuajiriwa kutumika pamoja na KDF au vinginevyo katika ulinzi wa taifa ima ndani au nje ya nchi". Viongozi wa CORD hivi karibuni wametuhumu utawala wa Jubilee kwa madai ya kujaribu kuiaanda NYS kijeshi lakini wakapuuzwa kwa kudaiwa kuwa na wivu kwa kazi nzuri vijana walikuwa wakifanya katika vitongoji duni! Ni kawaida viongozi kuunda wanamgambo kwa jina la vijana wa chama au kwa swala hili, kusingizia kuwawezesha vijana ambao wanaweza kutumika kwa haraka kusababisha vurugu. Maandamano mjini Nairobi mnamo Juni 22 na vijana kuunga mkono miradi ya NYS na maandamano pinzani yaliyofuatia mnamo Juni 23 katika mitaa ya Kibera dhidi ya miradi hiyo ni utangulizi wa kile tunatarajia kuwa mwanzo wa mbinu hii.

Mswada huu unampa Rais uwezo wa kuongeza mda wa kuhudumu kwa ofisi Mkuu, Makamu Mkuu na Makamanda wa KDF kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja na pia inataka kupanua umri wa kustaafu wa Mkuu wa KDF kutoka miaka 62 hadi 64. Hii ni kimsingi kiashiria kwamba usalama wa Nchi unategemea watu binafsi badala ya taasisi. Jambo ambalo lapelekea mda wa kuhudumu kuongezwa kwa vile hakuna warithi. Jakoyo Midiwo, Mbunge wa Gem alinukuliwa akisema "Serikali inajenga nafasi ya Usalama wa Nchi kupitia mlango wa nyuma ili kurudisha kazini Mkuu wa Jeshi aliyestaafu Julius Karangi. Hii haikubaliki" na kushutumu serikali kujaribu kuanzisha serikali ya kijeshi. Katika kipindi cha NTV cha Watu na Siasa kilichopeperushwa hewani Agosti 10, 2015, wazungumzaji walielezea kuhusu serikali ya Uhuru kwa taratibu kugeuzwa kijeshi kwa kutarajia uwezekano wa kuanzisha mabadiliko ya muhula wa Rais ambao kiwango chake ni vipindi viwili vya miaka mitano. Huu umekuwa mtindo na Marais wa kiafrika kukimbilia kubadili sheria kwa ajili ya kuruhusu utawala bila kiwango cha mda kuwekwa na Burundi, Rwanda na Uganda ni mfano mzuri. Jeshi ama wanamgambo  wanalengwa kutumika hapa ikiwa raia hawataki kufuata matakwa ya walio mamlakani.

Mswada huu pia unaondoa sharti la KDF kutangaza nafasi kwa mujibu wa majimbo. Nia ya kifungu hiki ni wazi kwa watu wote kwamba kinajaribu kuhakikisha kuwa wengi wa walio katika jeshi wanatoka maeneo ya Rais. Wanatarajiwa kutegemewa kwa kutumiwa ikiwa hali itajitokeza ambapo uongozi wa aliye kwenye mamlaka unapata tishio kutoka kwa wapinzani. Pia unakinga shughuli za KDF, ikiwa ni pamoja na matumizi ya bajeti yake na kazi yake kutokana na uchunguzi wa umma kwa kunyima Bunge jukumu la uhasibu. Ingawa bunge pia ni pango la rushwa na kwa hivyo si taasisi ya kuthaminiwa kufanya uhasibu, inatarajiwa kwamba uchunguzi wa umma kuhusu matumizi ya KDF ni muhimu sana ikizingatiwa wao ni walipa kodi. Waandaalizi wa mswada huu ni wazi nia yao ni kujificha nyuma ya pazia la 'Kandarasi za Kiusalama' ili kuficha njama zao.

Kutokana na uchambuzi juu ya matukio yanayozunguka mapendekezo ya mswada huu, inaweza kuonekana kwamba usalama na rushwa waenda sambamba katika nchi za Kibepari. Na haijawahi kuwa lengo ni kuhifadhi nchi badala yake ni kuhifadhi maslahi ya pamoja ya tabaka la wanasiasa na mabwenyenye. Utawala huu umejifunza kwa haraka kutoka kwa mabwana zake katika nchi za Magharibi kwamba serikali kufanikiwa ni lazima kubuni migogoro na kisha kusingizia baadae uwezo wa kutatua. Baada ya kukosea katika kila operesheni ya usalama iliyofanywa tangu operesheni 'Linda Nchi', serikali ilianza safari ya kujenga hali ya kudumu katika mizozo katika mabongo ya wananchi kwa matumaini kwamba wataunga mkono miswada kama hii ambayo kiujanja ina lengo la kuwanyamazisha. Ni wazi kuwa Serikali imeshindwa na jukumu lake la kutoa ulinzi kwa wananchi wake kutokana na kushindwa kubadilisha kimuundo vyombo vya usalama. Kwa bahati mbaya, hii inaonekana kufanywa kimakusudi kwa vile Shilingi billion 74 zilizotengwa katika bajeti kwa ajili ya jeshi ni kivutio kikubwa kwa magenge ya ufisadi.

Kwa kumalizia, Uislamu hautoi mda kwa Khalifa kuhudumu na kukaa kwake katika mamlaka haihusiana na kuungwa mkono na jeshi lakini kwa kuzingatia shariah. Kupitia thakafa ya kina kwa raia, serikali ya Kiislamu huhakikisha kwamba kila mmoja anaelewa jukumu lake katika jamii. Ni hofu ya kuhisabiwa na Muumba na ummah kwa ujumla ndio inafanya viongozi katika serikali ya Kiislamu kupeleka mambo yao kwa manufaa ya ummah. Kwa kuwa hakuna serikali ya Kiislamu, ni wajibu juu ya umma kuwa macho dhidhi ya njama za serikali hizi za kikafiri ambazo hutunga sheria zinazoweza kuzuia kusimamishwa kwa serikali ya Khilafah.

No comments: